CHAMA CHA WANANCHI CUF KUANZA MKUTANO WAKE MKUU HII LEO. WAJUMBE WATAKAOKOSA NAFASI ZA UONGOZI WAPEWA NENO.

Wakati Chama Cha Wananchi CUF kikiingia katika uchaguzi Mkuu Taifa kuanzia leo tarehe 23/06/2014, Viongozi wakuu wa Chama hicho wamewataka wajumbe watakaokosa nafasi za uongozi kutobabaika, na badala yake waendelee kukijenga chama hicho.
Akizungumza
katika hafla maalum ya kuagana na wajumbe wa Baraza Kuu pamoja na watendaji
wengine wa ngazi mbali mbali, Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif
Hamad, amesema kila mwanachama ana wajibu wa msingi wa kukijenga chama bila
kujali wadhifa alionao.
“Wasiorudi
kwenye baraza kuu na ngazi nyengine yeyote ya uongozi bado wana mchango mkubwa
wa kukijenga chama chetu ili kiweze kushika dola mwaka 2015, na jukumu hilo
limo ndani ya katiba ya chama chetu”, alisisitiza Maalim Seif katika hafla hiyo
iliyofanyika nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba
katika eneo la Kunduchi Dar es Salaam.
Amewapongeza
pia wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi kwa mashirikiano waliyokuwa nayo katika
kipindi chote cha miezi 64, hali ambayo amesema imeleta mafanikio makubwa ndani
ya chama hicho.
Maalim Seif
amesema ndani ya kipindi hicho Chama pia kilikabiliwa na changamoto mbali mbali
ambazo hata hivyo kwa kutumia busara na hekima za viongozi waliweza
kuzitatua. Amewasisitiza wajumbe
watakaochaguwa kuendeleza umoja na mshikamano uliopo, ili kuweza kufikia
malengo waliyojiwekea ya kukamata hatamu za dola katika uchaguzi mkuu
ujao.
Mapema akizungumza katika hafla
hiyo, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ambaye anakabiliwa na
upinzani katika uchaguzi huo, ameahidi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo,
na iwapo atashindwa ataendelea kukiunga mkono chama hicho kwa kutoa kila msaada
unaostahiki kwa maendeleo ya chama.
“Mimi
nikiangushwa katika uchaguzi nitaendelea kuwa mwanachama na kutoa mchango wangu
wote kwani suala hili la kugombea nafasi ni haki ya kikatiba kwa wanachama
wote” alieleza Prof. Lipumba na kuongeza,
“Nilikuwa
mwanachama wa kawaida kwa kipindi kirefu ndipo ikafika wakati chama kikaniteua
kugombea na kuchaguliwa Mwenyekiti hadi leo, kwa hivyo haki hii anaweza kuwa
nayo mwanachama yeyote”, aliweka bayana Prof. Lipumba.
Jumla ya
wagombea watatu wamejitokeza kugombea nafasi ya Uenyekiti Taifa akiwemo
Mwenyekiti wa sasa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba. Wagombea wengine wa nafasi
hiyo ya Mwenyekiti Taifa ni M’bezi Adam
Bakar kutoka Temeke Dar es Salaam na Chifu Lutalosa Yemba kutoka
Shinyanga.
Nafasi ya
Makamu Mwenyekiti ina mgombea mmoja ambaye ni Mhe. Juma Duni Haji na Ukatibu
Mkuu ni Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad. Aidha Prof. Lipumba ametumia fursa hiyo
kuwaeleza wajumbe kuwa bado chama hicho kinaendelea na juhudi zake ili kuweza
kupata katiba ya wananchi, katika mchakato wa katiba mpya unaotarajiwa
kuendelea tena mwezi Ogasti, 2014.
Katika hatua
nyengine Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Machano Khamis Ali, amesema
ameamua kwa hiari yake kutogombea tena nafasi hiyo kutokana na sababu mbali
mbali zikiwemo sababu za kiafya.
“Mimi
nimeamua kuwa mfano ndani ya chama chetu, sitaki kuwa king’ang’anizi wa nafasi
hii, nimeona nisigombee tena nafasi hii kutokana na sababu nilizozieleza,
lakini nakuahidini kwamba sitokwenda chama chengine na nitaendelea kutoa
mchango wangu wote katika kukijenga na kukiendeleza Chama chetu”, aliweka wazi
Mhe. Machano.
Mapema
akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza Kuu na watendaji wengine
wa Chama hicho, Bibi Najma Khalfan
amewatanabahisha viongozi na wanachama kuungana ili waweze kupata ushindi
katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Na: Hassan Hamad Dar.
No comments: