LIVE STREAM ADS

Header Ads

JESHI LA ZIMA MOTO MKOANI MWANZA LAPOKEA MSAADA WA VIFAA VYA UOKOAJI.



Jeshi la Zimamoto Mkoani Mwanza, limepokea msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh 2,000,000 kutoka nchini Ujerumani na Finland kwa ajili ya shughuli zake za uokoaji.

Kikosi hicho ambacho
kinakabiliwa na changamoto mbalimbali, kimekabidhiwa buti jozi sita, jaketi (12), makoti (15), suruali (22), kofia ngumu (10), kofia za kawaida (10), fulana tano na ovaroli mbili kwa ajili ya utekeleza wa majukumu yake ya kikazi.

Akizungumzia vifaa hivyo, Kaimu Kamanda wa kikosi cha Zimamoto Mkoani Mwanza Inspekta Augustine Magere alieleza kwamba , kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu katika jiji la Mwanza, kikosi hicho bado kinakabiliwa na changamoto nyingi za  vifaa vya kutendea kazi.

Inspekta  Magere alieleza kwamba kwa sasa jiji hilo lina magari manne ya zimamoto ambapo kati ya hayo  mawili yapo uwanja wa ndege na mawili katikati ya jiji jambo ambalo halikidhi mahitaji kutokana na wingi wa watu waliopo Jijini Mwanza huku matukio ya moto yakitokea mara kwa mara hususani katika maeneo ya nje ya jiji.

“Tunakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya kutendea kazi, lakini tuliwasiliana na marafiki zetu wa Wurzburg nchini Ujerumani na Tampere nchini Finland ili waweze kutusaidia ambapo leo hii wametusaidia baadhi ya vifaa.” Alisema Magere.

Magere alisema hayo wakati akikabidhiwa vifaa na mwakilishi wa afisa uhusiano wa jiji la Wurzburg, Idd Hussein vilivyotolewa na jiji jilo rafiki la Wurzburg lililopo nchini Ujerumani.

Naye Hussein aliyekabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya jiji la Warzburg, alisema lengo kubwa la kutoa vifaa hivyo ni kukiboresha kikosi hicho ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

“Wamefanya hivyo ili kuboresha mahusiano, elimu ya utendajio kazi pamoja na kuboresha idara hiyo ya zimamoto katika jiji letu,” alisema Hussein.

Nae Askari wa kikosi hicho cha Zima Moto Mkoani Mwanza koplo Lucy Nginila alisema kupatikana kwa vifaa hivyo kutawasaidia kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa hasa katika uokoaji wa watu na mali zao.
Na Prisca Japhes: Mtanzania Media-Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.