WANANCHI WA LUCHELELE JIJINI MWANZA WACHACHAMAA JUU YA HATMA YA ARDHI YAO. WAPANGA KUKUTANA KESHO.
Kutokana
na tatizo kubwa la migogoro ya ardhi Jijini Mwanza kukithiri katika maeneo
mbalimbali, wananchi wa eneo la Luchelele Jijini hapa, wamesema hawako tayari
kunyanyaswa mpaka kieleweke.
Hatua hii imekuja baada ya Halimashauri ya Jijiji la Mwanza kutoa taarifa kwa wakazi wa eneo hilo
inayoelekeza kwamba baadhi ya maeneo yaliyopo katika eneo hilo yanatakiwa kuwekwa wawekezaji kwa ajili ya
maendeleo ya Jiji la Mwanza.
Mgogoro huo unaoendelea eneo la Luchelele kata ya Mkolani Wilayani
Nyamagana , umekuwa kitendawili hadi sasa kutokana na baadhi ya wananchi
waliochukuliwa maeneo yao kudai kuwa muafaka hauta patikana mpaka walipwe fidia
inayolingana na maeneo yao yaliyochukuliwa na halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Mgogoro huo ulioanza tangu mwaka 2006 na kutegemewa kumalizika mwaka 2011, lakini
hadi sasa hali ni tete kwa wakazi waishio maeneo hayo ambapo swala hilo bado
halijapatiwa ufumbuzi huku baadhi ya maeneo yakidaiwa kujengwa na baadhi ya
Viongozi wa Jiji la Mwanza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
juzi, wakazi wa maeneo hayo walisema kuwa tatizo hilo limeanza muda
mrefu na hadi sasa hawaelewi litaisha lini na hakuna taarifa yoyote wanayoipata
kutoka kwa viongozi wa juu.
‘’Hatujaona chochote kinachoendelea hapa Luchelele sisi hatuondoki
kwa sababu tangu watuambie watatulipa fidia zetu ili tupishe ardhi hii hawajafanya hivyo, sasa twende tukakae
wapi na hata hizo fidia wanazosema watulipe hazilingani na maeneo yetu’’.
Alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Aliongeza kuwa pamoja na
kuchagua mwakilishi atakaye wasilisha hoja zao kwa uongozi wa halmashauri ya
Jiji la Mwanza kwa ajili ya migogoro hiyo, hakuna taarifa yoyote muafaka juu ya
ardhi yao na kudai kuwa hawataondoka katika maeneo hayo hadi pale swala hilo
litakapo kamilika.
‘’Huyu mwenyekiti wa
mgogoro tumemchagua sisi lakini sasa ametugeuka na kuwa adui yetu, hatuambii chochote
kinachoendelea huko Jijini, wala hatupati taarifa yeyote sasa sisi hatuondoki
hata kwa ngumi’’alisema mkazi huyo.
Wengine walieleza kwamba hawakatai
kupisha katika eneo hilo kwa ajili ya maendeleo, isipokuwa wanachokitaka
wao ni kupewa ruhusa ya wao kuendelea kujenga katika viwanja vyao kwani
walizuiliwa na halmashauri kutofanya shughuli za ujenzi kwa wale wanaojenga
hadi pale watakapo pewa taarifa kutoka jiji Mwanza.
Kutokana na hali hyo wananchi hao wamepanga kufanya mkutano wao
utakao fanyika leo Jumamosi wakiongozwa na Mwenyekiti wa mtaa wa Luchelele kati,
Vicent Lusana na hivyo kuwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi katika kikao hicho kitakachofanyika shule ya msingi Luchelele ili
kujadili muafaka wa mgogoro hu unao wakabiri.
Akizungumzia swala hili kwa njia ya simu, Meya wa jiji la Mwanza Stanslaus
Mabula alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kudai kuwa ulikuwa umefikia mwisho
lakini umeibuliwa na wanasiasa kutokana na kwamba kuna baadhi ya watu
wanaotumia mgogoro huo kwa njia ya kujinufaisha kisiasa na kuwatumia wananchi
kuwachochea kufanya maandamano yasiyo na tija.
Aliongeza kuwa tarehe 3 Septemba
utafanyika mkutano katika eneo hilo kwa lengo kujadili namna ya kutatua
mgogoro huo ili kuruhusu wananchi wanaomiliki ardhi katika eneo hilo la
Luchelele kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Na Prisca Japhes: Mtanzania Media-Mwanza.
No comments: