LIVE STREAM ADS

Header Ads

WASICHANA WANAOISHI MITAANI JIJINI MWANZA WALIA NA VITENDO VYA UNYANYASI KUTOKA KWA MAASKARI WA DORIA.

Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. Namsemba Mwakatobe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa wasichana wanaoishi mitaani jijini Mwanza. Kwa tukio lolote la ukatili na unyanyasaji TUMA MSG kwenda namba 0682 72 90 07, AU PIGA SIMU DAWATI LA JINSIA-MWANZA 0755 92 92 24 00.

Wasichana wanaoishi Mitaani Jijini Mwanza wamewalalamikia baadhi ya Maaskari Polisi na polisi jamii wanaofanya doria katikati ya Jiji nyakati za usiku, kutokana na
manyanyaso wanayowapa pindi wanapowakuta wamelala vibarazani.

Hayo yamebainishwa jana na Wawakilishi wa Wasichana wanaoishi Mitaani katika Kikao na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, kilichoandaliwa na Mtandao wa Watoto na Vijana Mkoani Mwanza unaofahamika kama Mwanza Youth and Children Network (MYCN). Kikao hicho kiliandaliwa kupitia mradi wake wa Jiji langu Sauti Yangu.

Wakizungumza katika Kikao hicho Wasichana hao walibainisha kwamba wamekuwa wakipata manyanyaso makubwa ikiwa ni pamoja na kuombwa rushwa ya pesa na ngono kutoka kwa baadhi ya maaskari polisi na Polisi jamii ambao wamekuwa wakifanya doria katikati ya Jiji la Mwanza pindi wanapokutwa wamelala vibarazani na kuwakamata kwa madai kwamba wamekuwa wakijiuza Mitaani.

Wasichana hao waliendelea kueleza kuwa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali pindi wawapo mitaani lakini wamekuwa wakikosa usaidizi pindi wanapofika hata katika vituo vya polisi kwa ajili ya kuripoti matukio ambayo yamekuwa yakiwasibu kwa madai kwamba wamekuwa hawapati msaada kwa dhana ya kwamba wao ni watoto wa mitaani na wamekuwa wakijiuza pindi wawapo mitaani.

Pia walibainisha kuwa rushwa ya ngono ambayo wamekuwa wakiombwa na baadhi ya maaskari imekithiri mitaani pindi wanapokamatwa nyakati za usiku, jambo ambalo walisema limekuwa likiwaathiri kwa kuwa hadi sasa baadhi yao wameambukizwa magongwa ya ngono ikiwemo virusi vya Ukimwi sanjari na kupatiwa mimba jambo ambalo linazidi kuongeza idadi ya watoto wanaoishi mitaani.

Akijibu Malalamiko ya Wasichana hao kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi ASP. Namsemba Mwakatobe amekiri kuwa malalamiko yanwasichana hao yanaweza kuwa ni ya kweli ama laa, hivyo jeshi la polisi litahitaji ushirikiano wao kwa ajili ya kuwabaini askari wake ambao wanakiuka maadili ya kazi yao kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Ili kuondokana na changamoto wanazokutana nazo mitaani, ASP.Mwakatobe aliwasihi wasichana hao sanjari na watoto wengine wanaoishi mitaani kurejea katika familia zao kwa kuwa kila mtoto alie mtaani ana chimbuko la familia yake huku akiwasihi wale ambao hawana ndugu wa karibu kabisa wa kuwasaidia kutulia katika vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwa baadhi ya watoto wamekuwa wakitoroka katika vituo hivyo kwa ajili ya kuingia mitaani na kuwa omba.
Shaban Ramadhan-Mwenyekiti MYCN (Kushoto) akiwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. Namsemba Mwakatobe.
Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. Namsemba Mwakatobe.
Brightius Titus-Katibu Mkuu MYCN.
Rebeca Richard, Mwanafunzi wa Field-MYCN.
Wawakilishi wa Wasichana wanaoishi Mitaani wapiwa katika Kikao baina yao na Mrakibu Msaidizi wa Polisi kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana.
Wawakilishi wa Wasichana wanaoishi Mitaani wapiwa katika Kikao baina yao na Mrakibu Msaidizi wa Polisi kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana.
Mwanahabari Mtoto kutoka Baraza la Watoto Mkoani Mwanza akichukua Matukio yaliyokuwa yakiendelea katika Kikao cha Wawakilishi wa wasichana wanaoishi Mitaani na Jeshi la Polisi. Kubwa zaidi ilikuwa kujadili changamoto wanazokumbana nazo mitaani kutoka kwa Wanausalama na namna ya kukabiliana nazo.
Shaban Ramadhan-Mwenyekiti MYCN.
Na: George Binagi @99.4 Metro FM & Mtanzania Media.

No comments:

Powered by Blogger.