DC MPYA KINONDONI MH.PAUL MAKONDA ASEMA ATAONGOZA KWA KUFUATA SHERIA NA SI MIHEMUKO YA KISIASA.
Na: George Binagi-GB Pazzo.
Siku
moja baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Jakaya
Kikwete, Mkuu Mpya wa Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es salaam Mh.Paul Makonda
amewaondoa wananchi hofu kwa kusema kuwa uongozi wake utasimamia kanuni,
taratibu na sheria na siyo mihemko ya kisiasa kama wengine wanavyonadhia.
Mh.Makonda alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na 99.4 Radio
Metro Fm ya Jijini Mwanza kwa njia ya simu, akielezea namna alivyopokea uteuzi
wake sanjari na kuzungumzia mijadala mbalimbali iliyoibuka katika mitandao ya
kijamii kufuatia uteuzi wake.
Mh.Makonda ambae kabla ya utauzi huo alikuwa ni Katibu wa Hamasa wa
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, alisema kuwa jambo la
kwanza anamshukuru Rais Kikwete kwa kumuamini na kumuteua kuwa msaidizi wake
katika Wilaya ya Kinondoni huku pia akiwashukuru Watanzania waliomuombea na
kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali na hatimae
kuonekana anafaa kuwa kiongozi Serikalini.
“Haki ni tofauti na dhambi. Ukiwa na dhambi hofu itakutawala. Ukiwa na
haki ujasiri ni sehemu ya maisha yako. Asie kuwa na hatia na asonge mbele
katika utendaji wake wa kazi. Alie na hatia hofu ndiyo itakayomtafuna. Kwa
nafasi tuliyopewa tunakwenda kuifanya kazi kwa mjibu wa sheria, taratibu na
kanuni.
Sasa sitegemei uwe na hofu wakati taratibu unazijua, sheria unazijua na
kanuni unazijua”. Alisema Makonda wakati akijibu hoja kwa wanaodhania uongozi
wake utagubikwa na mihemuko ya kisiasa.
Pamoja na mambo mengine pia Makonda alihitimisha kwa kusema kuwa
hakuna Tanzania bila Mtanzania na hakuna Mtanzania bila Tanzania hivyo
Watanzania hususani vijana watimize majukumu yao vyema kwa ajili maendeleo ya
Taifa ambapo alishauri kuwa huu ni wakati wa kujituma, kujifunza na kubadilika
na siyo wakati wa kujadili vitu au watu ambapo aliwahimiza zaidi wazee pamoja
na viongozi mbalimbali wa dini kuendelea kuliombea Taifa ili lidumu katika
Amani, Umoja na Utulivu kwa faida ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Juzi Februari 18 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mh.Mizengo Pinda aliweka wazi uteuzi wa Wakuu wa Wilaya uliofanywa na Rais Kikwete
ambapo uteuzi huo uliwang’oa madarakani wakuu wa wilaya 19 na kuwateua wapya 27
sanjari na kuwahamisha 64 huku 42 wakibaki kwenye vituo vyao vya kazi.
Muda mfupi baada ya Uteuzi huo, ziliibuka hoja na Mijadala mbalimbali
hususani katika mitandao ya kijamii ambapo watu wengi walikuwa wakizungumzia
uteuzi huo ambao walikuwa wakiuelezea kuwa umeonekana kama Ahsante kutoka kwa
Rais Kikwete kwa baadhi ya Wakuu wa Wilaya wapya kutokana na harakati zao za
kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM.
No comments: