LIVE STREAM ADS

Header Ads

WANANCHI WA KAWAIDA WASHINDWA KUPATA NAKALA ZA KATIBA MPYA JIJINI MWANZA.

Edwin Soko (Kulia) ambae ni Mkurugenzi Mtendaji kutoka Taasisi ya Kuchochea Utawala Bora na Uwazi nchini Tanzania.
Na:George Binagi-GB Pazzo.
Imeelezwa kuwa zoezi la ugawaji wa Nakala za Katiba Mpya limekuwa la kusuasua kwa wananchi wa Kawaida Jijini Mwanza, kutokana na hali halisi kuonyesha kwamba watu kutoka katika mashirika na taasisi mbalimbali ndio wanaonufaika na zoezi hilo.

Hayo yalielezwa jana Mkoani Mwanza na Edwin Soko ambae ni Mkurugenzi Mtendaji kutoka Taasisi ya Kuchochea Utawala Bora na Uwazi hapa nchini, wakati akizungumza na Waandishi wa habari juu ya mwenendo wa ugawaji wa Nakala za Katiba Mpya Jijini Mwanza.

Soko alisema kuwa mpaka sasa mwenendo wa ugawaji wa nakala za katiba mpya si wa kuridhisha kwa kuwa nakala za katiba inayopendekezwa hazijawafikia wananchi waliowengi ambapo fomu zilizotolewa na taasisi hiyo katika Ofisi za Kata katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela zinaonyesha kwamba waliopata nakala hizo ni wale wanaotoka katika taasisi ama Mashirika mbalimbali huku kukiwa hakuna nafasi hata moja iliyojazwa na mwananchi wa kawaida.

“Katika Jiji la Mwanza kwa maana ya Wilaya za Ilemela na Nyamagana, fomu zinaonyesha kwamba hakuna sehemu hata moja ambayo imejazwa na mwananchi wa kawaida. Fomu hizo zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wananchi waliopata Nakala za Katiba Mpya ni wale wanaotoka katika Mashirika au Taasisi mbalimbali”. Alisema Soko.

Kutokana na hali hiyo Taasisi hiyo imependekeza kwamba Serikali pamoja na watendaji wake waliopewa jukumu la kugawa nakala za katiba inayopendekezwa inapaswa kugawa katiba kwa wananchi wa kawaida ili kila mwananchi aweze kupata nakala yake badala ya kutoa kipaumbele kwa makundi, taasisi ama mashirika mbalimbali.

Hata hivyo Soko alitoa Ushauri kwa baadhi ya wananchi ambao tayari wamepata Nakala ya Katiba Mpya kujiwekea utaratibu wa  kukutana kwa pamoja katika vijiwe mbalimbali na kuisoma Katiba inayopendekezwa kwa lengo la kuielewa Katiba hiyo inayopendekezwa kabla ya kwenda kuipigia kura April 30 Mwaka huu.

No comments:

Powered by Blogger.