DIWANI KATA YA MKOLANI JIJINI MWANZA AAGIZA KUFANYIKA SENSA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA NGOZI.
Na: George Binagi-GB Pazzo
Diwani wa Kata ya Mkolani (CCM) Jijini Mwanza Stanslaus
Mabula amemwagiza Mtendaji wa Kata hiyo kwa kushirikiana na Watendaji wengine
wa Serikali za Mitaa, kufanya Sensa kwa watoto wenye ulemavu wa ngozi kwa lengo
la kuwaimarishia Ulinzi.
Mabula ambae pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza alitoa kauli
hiyo juzi kufuatia kukithiri kwa vitendo vya Utekaji na Mauaji kwa watu wenye
Ulemavu wa ngozi hapa nchini hususani katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema kuwa anasikitishwa na Vitendo vya Ukatili, Utekaji na
Mauaji kwa Watoto wenye ulemavu wa ngozi katika kipindi hiki cha kuelekea
katika Uchaguzi Mkuu, jambo ambalo linaongeza wasiwasi kwamba kuna baadhi ya
wanasiasa wanahusika katika kufadhiri vitendo hivyo.
“Mimi niseme tu binafsi nimepokea kwa masikitiko makubwa suala
hili. Hivi karibuni tumesikia Albino kule Kwimba ametekwa mpaka leo
hajapatikana. Albino Geita pale ametekwa na amepatikana akiwa marehemu na baadhi
ya viuongo vyake vimechukuliwa. Niseme tu mimi kama mwanasiasa lakini kama
binadamu mwingine na mwananchi wa kawaida kitendo hiki siyo kizuri, kinaumiza
sana na kinachukiza na hasa pale kinapoanza kuhusishwa na nyakati hizi za
Uchaguzi”. Alisema Mabula na Kuongeza,
“Sisi wanasiasa hatuwezi kufanana wote na wala siwezi kusema
hapana au ndiyo, inawezekana tafiti zinaonyesha wapo watu wanatumia mbinu hizo
za kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi lakini mimi niseme tu siyo jambo zuri
maana hata mwanasiasa unaeshinda kwa kumuua mwanadamu mwenzako kisa tu ualibino
wake siku moja mwenyezi Mungu atakupa uongozi wa adhabu ambao daima huwezi
kuufurahia katika Maisha yako”.
Kufuatia hali hiyo Mabula alibainisha kwamba pamoja na kwamba jeshi
la polisi linafanya kazi kubwa ili kuhakikisha linawalinda watu wenye ulemavu
wa ngozi, pia yeye kama Diwani wa Kata ya Mkolani amemwagiza Mtendaji wa Kata
hiyo kwa kushirikiana na watendaji na Wenyeviti wa Mtaa kuhakikisha kwamba
wanapita katika kila Kaya na kutambua walipo watoto wenye ulemavu wa ngozi kwa
lengo la kuwaimarishia ulinzi ili kuongeza wigo na upana wa maisha yao kadri
Mungu alivyowapangia.
Hivi karibuni katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kumeibuka Vitendo vya
Utekaji na Mauaji kwa watoto wenye Ulemavu wa ngozi jambo ambalo limeushtua
ulimwengu mzima ambapo mwishoni mwa mwezi Januari akizungumza Mkoani Mwanza, Peter
Ash ambae ni Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za watu wenye Ulemavu wa ngozi
(Under The Same Sun) lenye Makao yake Makuu nchini Canada aliitaka Serikali
kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote wanaotajwa kufadhiri vitendo vya
Utekaji na Mauaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ambapo aliwatupia lawama
baadhi ya Wafanyabiashara na Wanasiasa kuhusika katika kufadhiri vitendo hivyo.
Itakumbukwa kuwa Disemba 27 mwaka jana mtoto mwenye ulemavu wa
ngozi Pendo Emmanuel (4) Mkazi wa Kwimba Mkoani Mwanza alitekwa na watu
wasiojulikana na mpaka sasa hajulikani alipo huku tukio kama hilo likijrudia
tena Februari 15 mwaka huu katika Kijiji cha Ilelema Mkoani Geita ambapo mtoto
mwenye ulemavu wa ngozi Yohana Bahati (1) alitekwa akiwa amebebwa na mama yake mzazi
na baada ya siku mbili akapatikana akiwa tayari ameuawa huku baadhi ya viuongo
vyake vya mwili vikiwa vimekatwa. Katika tukio hilo wavamizi hao walimjeruhi
vibaya kwa mabanga mama yake na Yohana wakati akijaribu kumuokoa mwanae.
No comments: