NI MIAKA SABA SASA TANGU UTUTOKE DUNIANI. TUNAKUKUMBUKA SANA BABA YETU MPENDWA.
![]() |
Mwanao GB bado nakukumbuka. |
Ilikuwa ni Sekunde, Dakika, Masaa, Siku,
Wiki, Mwaka hatimae hivi sasa ni miaka imepita tangu ututoke duniani Baba yetu
Mpendwa, huku ukiacha kilio na majonzi kwa wanao tuliokuwa bado wachanga ambao
hakika ulituacha ilihali tukihitaji malezi yako.
Ukiwa na Miaka 83
mwaka 2008, Mzee wetu Mzee Daniel Marwa Binagi Mzaliwa na Mkazi wa Kitongoji
cha Chira Kata ya Turwa (Zamani), hivi sasa Kata ya Kenyamanyori Wilaya ya
Tarime Mkoani Mara Mwenyezi Mungu alikupenda zaidi na kukuchukua ili ukapumzike
baada ya kuteseka kwa maradhi katika kipindi cha muda mrefu.
Hakika uliipenda
na kuiongoza Familia yako bila ubaguzi wa aina yoyote. Ulionyesha Mapenzi tele
si tu kwa Wanao, Wajukuu zako, Wake zako bali kwa kila mmoja aliekuzunguka ambapo
uliweza kuonyesha mapenzi tele kwake huku tabia yako ya kuchukia upuuzi na
kuukumbatia ukweli ukikuongezea sifa rukuki kwa waliokufahamu.
Ukiwa na Elimu ya
darasa la nne ambayo uliipata enzi za Mkoloni, uliweza kuleta mapinduzi ya
ajabu katika Kijiji chako na hata Wilaya ya Tarime na kuwa mmoja wa Watu wenye
Mafanikio makubwa Wilayani Tarime si tu kwa Kuwekeza katika Ujenzi wa nyumba na
Biashara katika mji wa Tarime bali hata katika Uungwana wako.
Ulijizolea sifa
ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kadri apendavyo na hivyo ndivyo
ilivyokuwa na ndiyo maana wakapatikana vijana mbalimbali kutoka katika uzao
wako wakiwa nafasi mbalimbali za utumishi ikiwa ni pamoja na wale walioingia
katika Sekta ya Elimu, Afya, Habari, Biashara, Urubani ikiwa ni miongoni mwa
taaluma mbalimbimbali huku wewe mwenyewe ukiamini katika mfumo wa Biashara,
Kilimo na Ufugaji.
Hakika wote
waliopata malezi yako wanajivunia mpaka leo kuwa na Mzazi kama wewe Mzee wetu Daniel
Marwa Binagi. Nakumbuka mambo mengi sana kutoka kwako ambayo ulikuwa
ukiwatendea wakati huo mimi nikiwa mdogo. Nilitamani sana kupata malezi yako
lakini Mwenyezi Mungu alikupenda zaidi. Nakumbuka namna ndugu zangu walivyosoma
katika Shule na Vyuo vizuri tena kwa gharama kubwa. Naogopa kusema sana ili
nisije nikakufuru ila nina kila sababu ya kusema kwamba pengine nami ningekuwa
mmoja wa wanao ambao wangesoma katika shule na vyuo vizuri kama ulivyokuwa
ukiniahidi wakati ukiwa kitandani unauguza maradhi yaliyokuwa yakikusibu.
Hakika Mzee wetu
wetu Daniel Marwa Binagi tututaendelea kukukumbuka kwa kuyaendeleza yale yote
mazuri uliyotuachia licha ya changamoto nyingi zinazojitokeza kutokana na pengo
lako. Yapo mengi ya kusema ila kwa leo nasema kwamba pengo uliloliacha tangu
tarehe 06.02.2008 bado linaonekana na halitasahaulika kamwe. Hakika safari uliyoianza
hapa duniani tangu tarehe 25.02.1925 ilifikia tamati mwaka huo wa 2008. Mwenyezi
Mungu Ailaze Roho yako Pahala Pema Peponi, Amina! Ni mimi mwanao Mpendwa George
Marwa Binagi.
No comments: