LIVE STREAM ADS

Header Ads

UVCCM TAIFA WAITIKISA HALMASHAURI YA WILAYA YA IKUNGI MKOANI SINGIDA.

Kaimu Katibu Mkuu UVCCM  Taifa, Shaka Hamdu Shaka, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Puma iliopo Wilaya ya Ikundi mkoani Singida.
Na Fahadi Siraji, Singida 

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM, kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu wake, Shaka Hamdu Shaka, umeitaka halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kutenga bajeti ya dharura itakayofanikisha mradi wa maji safi kufika katika shule ya sekondari Puma iliopo wilayani humo.

Aidha Umoja huo umeisisitiza kwamba halmashauri hiyo katika upangaji wa bajeti zake, unapaswa kuyapa kipaumbele masuala ya msingi ambayo ni muhimu kwa maisha ya jamii ikiwemo utatuzi wa kero za afya.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya shule ya sekondari Puma wilayani humo, mwanafunzi Mariam Gwau anayesoma kidato cha nne, alielezea tatizo la barabara na umbali kutoka mahali wanakoishi hadi kufika  shuleni  ni hatarishi kwao kiusalama.

Pia alisema kukosekana kwa maji safi na salama kwao ni shida inayowapa msongo wa mawazo kwa sababu wanateka maji machafu katika bwawa moja wanalochangia pamoja na mifugo.

"Mimi na wanafunzi wenzangu sasa tunakaribia kumaliza  masomo yetu ili tufanye mtihani wa kuelekea kidato cha tano, tuna mwaka mmoja sasa hatujafundishwa somo la fizikia, kwetu hii ni sawa na kutukatisha tamaa kwa maendeleo ya elimu yetu"Alisema Maryam.

Mwanafunzi mwingine anayesoma wa kidato cha tatu, Angelina Amani, alimueleza Kaimu Katibu Mkuu UVCC Taifa, Shaka Hamdu Shaka, kwamba shuleni hapo hakuna umeme, maabara haijamalizika huku pia kukiwa hakuna vifaa vya kufundishia kwa vitendo jambo ambalo linawasikitisha sana na kuwa kikwazo kikubwa katika masomo yao.

Akijibu hoja hizo, Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Abel Sury, alisema upo mradi wa maji safi lakini kwa mwaka wa fedha 2016 /17 mpango wa kufikisha maji katika  shule hiyo  haupo na kwamba jengo la maabara likifikia hatua ya linta halmashauri itasaidia kukamilika kwake.

Matamshi hayo ya Makamu Mwenyekiti hayakuonekana kumridhisha Shaka, ambaye alimtaka Makamu huyo Mwenyekiti kuhakikisha maji yanafika sekondari hiyo ya Puma haraka iwezekanavyo. 

Baada ya hapo, Shaka aligonga hodi katika ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mohamed Nkya, na kufanya nae mazungumzo ambapo alimisitiza kutenga bajeti ya dharura ili kuhakikisha maji safi yanafika katika shule hiyo. 

Shaka alimulekeza Mkurugenzi huyo kuwa masuala yanayohusu huduma za jamii yanapaswa kuwekewa umuhimu mkubwa na kupatiwa suluhisho la kudumu kabla hayajawa majipu na kero zinazokatisha juhudi za wananchi hasa wanafunzi wanaotakiwa kupata elimu bora, ambapo mkurugenzi huo alionekana kukubaliana na ushauri huo wa Shaka.
Kaimu Katibu Mkuu UVCCM  Taifa, Shaka Hamdu Shaka, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Puma iliopo Wilaya ya Ikundi mkoani Singida.
Mariam Gwau ambae ni mwanafunzi wa kidato cha kidato cha nne, Shule ya Sekondari Puma mkoani Singida, akizungumzia kero na changamoto zinazowakabiri wanafunzi katika shuleni hiyo.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Mohamed Nkya, akiwa katika mkutano na Kaimu Katibu Mkuu UVCCM Taifa na ujumbe wake.

No comments:

Powered by Blogger.