LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Biteko akutana na wawekezaji mradi wa uchimbaji wa Uranium

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com

Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akisalimiana na Mkurugezni Mkuu wa kampuni ya Uranium One Holdings N.V, Vladimir Hlavinka (kushoto), baada ya kuwasili ofisini kwake kwa mazungumzo. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra, Fredrick Kibodya.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia) akimsikiliza Makamu wa Rais wa kampuni ya Uranium One Holdings N.V, Vladimir Hlavinka akielezea nia yao ya kutaka kuwekeza katika sekta ya madini nchini wakisubiri uwekezaji wao katika masuala ya uranium uliositishwa kwa muda.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra, Fredrick Kibodya akichangia mada katika kikao baina ya wizara na kampuni ya Uranium One Holdings N.V ofisini kwa waziri jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa kwanza kulia) akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Uchumi wa Kampuni ya Uranium One Holdings N.V Alexander Ryabchenko akiwasilisha hoja mbele ya waziri juu ya nia ya ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini.Kulia ni kamishina wa Madini nchini David Mlabwa.
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mantra, Fredrick Kibodya, akifuatiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Augustine K. Ollal mwishoni ni Msaidizi wa Waziri Kungulu K. Masakala.
Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wawekezaji kutoka kampuni ya Uranium One Holdings N.V waliofika kuzungumzia nia yao ya kuwekeza katika maeneo mengine ya madini nchini.

Na Nuru Mwasampeta, Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya uranium katika mto Mkuju ulioko mkoani Lindi ya Uranium One kutokusita kuwasiliana naye pindi wanapokutana na changamoto katika utekelezaji wa mradi wao.

Aliyasema hayo jana katika kikao chake na watendaji wa kampuni hiyo kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma.

Aidha, Biteko alisema kuwa maombi yote ya leseni kubwa za uchimbaji wa madini zinawasilishwa katika baraza la Mawaziri ili kuweza kuridhiwa baada ya wawekezaji kuonesha nia na kuwasilisha maombi ya leseni hizo.

Biteko alikiri kuwa anao uelewa wa kile kinachoendelea katika uwekezaji huo kutokana na ushirikishwaji alioupata kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki kupitia vikao mbalimbali alivyoshiriki.

Akizungumzia lengo la ujio wao katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Uranium One, Frederick Kibodya alisema ni kuelezea maendeleo waliyofikia katika uwekezaji huo pamoja na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Madini.

Alisema, uteuzi huo umelenga katika kukuza sekta ya madini ikiwa ni pamoja na mradi wa uchimbaji wa madini ya uranium, “Tunaimani kubwa kwako na tunamshukuru Mungu kwa kukupa nafasi hii” alisema Kibodya.

Akizungumzia uwekezaji uliofanyika mpaka sasa katika mradi huo alisema ni kiasi cha dola za kimarekani Milioni mia mbili ($200mil) kutoka mradi ulipoanza mwaka 2009.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo Kibodya alisema ni pamoja na kusaidia katika kukuza teknolojia nchini. Alisema madini hayo yakichimbwa yanatumika katika kuzalisha umeme ambayo ni teknolijia mpya nchini.

Mradi utasaidia katika kuongeza ajira nchini. Aliendelea kufafanua kuwa kwa kipindi cha ujenzi wa mradi wanatarajia kuajiri watanzania 1600 kwa kipindi cha miezi kumi na nane.

Aidha, alibainisha kuwa kutakuwepo na uzalishaji wa ajila zisiso rasmi kiasi cha watu 4500 wakati wa ujenzi na 2300 pindi uzalishaji utakapoanza.

Alisema, mradi utasaidia katika kuhamisha utaalamu kutoka kwa wawekezaji kwenda kwa wazawa na mradi umelenga katika kutoa elimu ya ajira na utaalamu kwa wazawa.

Pia Kibodya alisema, mradi unatarajia kuliingizia taifa pato la kiasi cha dola za kimarekani milioni 220 kama kodi kwa mwaka, kiasi ambacho kitakuwa kikibadilika kadri uzalishaji unavyoongezeka.

Mradi wa uchimbaji madini ya uranium katika mto Mkuju unafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Mbia wa kampuni ya Mantra anayejulikana kama Rosatom.

No comments:

Powered by Blogger.