LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kilimo cha umwagiliaji suluhisho la mabadiliko ya tabia nchi

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Kiongozi wa skimu ya kilimo cha umwagiliaji cha Mkombilenga iliyopo wilayani Iringa katika Kanda ya Umwagiliaji ya Mbeya, Fundi Mihayo (kulia) akipokea kikombe kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) hapa nchini, Nahofumi Yamamula baada ya skimu hiyo kushika nafasi ya kwanza katika kongamano kubwa la kushindanisha vyama vya umwagiliaji lilofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba akitoa neno la kufunga kongamano hilo lililoshindanisha vyama wa umwagiliaji jijini Dodoma.
Majaji na washiriki wakiwa kwenye kongamano la siku mbili la kushindanisha vyama vya umwagiliaji lililofanyika jijini Dodoma.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la kimataifa la maendeleo la Japan (JICA) nchini, Nahofumi Yamamula (katikati) akiongea na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba (kushoto) baada ya mapumziko wakati wa kongamano la kushindanisha vyama vya umwagiliaji lilofanyika jijini Dodoma. Kulia ni Yoichi Yamauchi Mshauri kutoka mradi wa kuwajengea uwezo wakulima katika eneo la umwagiliaji.

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kunaweza kuwa ni njia sahihi ya kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. 

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba alipokuwa akifunga kongamano ya wakulima lililoandaliwa na shirika la Maendeleo la kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Mhandisi Futakamba alisema Serikali imeweza kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya Umwagiliaji na kuchukua jukumu kubwa la kutoa mafunzo ya matunzo ya miundombinu hiyo kwa wakulima, ili kuweza kukabiliana na athari na hasara zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, 

"Ili kuweza kufikia lengo hili ni lazima serikali na wakulima kwenda pamoja ili kufanikisha, hali ambayo inaweza pia kusaidia wakulima nao kuingia zaidi katika kilimo cha biashara kama vile wakulima wa skimu ya Lemkuna na Pawaga, pamoja na kuwa na uhakika wa chakula nchini" alisema Mhandisi Mbogo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Marco Ndonde alisema Tume hiyo imejipanga kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo benki ya kilimo na mashirika mbalimbali ya maendeleo.

"Sambamba na hilo Tume ina mpango wa kujenga mabwawa ili kufanya kilimo cha umwagiliaji kiwe  na uhakika wa kupata maji ya kutosha pamoja na kufungua miradi ya kilimo hicho kitakachoajiri vijana kutoka vyuo vikuu nchini" alisisitiza Ndonde.

Akiwasilisha mada katika siku ya mwisho ya kongamano lililoshindanisha vyama vya wamwagiliaji nchini, Fundi Mihayo ambaye ni kiongozi wa skimu ya umwagiliaji ya Mkombilenga iliyopo mkoani Iringa alisema lengo la Serikali kuwezesha wakulima kuuza mchele badala ya kuuza mpunga katika maeneo ya skimu za kilimo cha umwagiliaji limefanikiwa kwa kisia kikubwa kwani kwa sasa skimu nyingi zimeweza  kufunga mashine za kukoboa nafaka kama vile mpunga na kupaki katika madaraja na ujazo tofauti.

"Haya yote ni manufaa ya tokanayo na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa mafunzo kwa kushirikiana na serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA jambo ambalo limepelekea wakulima kuwa na soko la uhakika la zao la mpunga hasa baada ya Serikali kuhamia Makao Makuu ya  nchi Dodoma, wakulima wa skimu ya umwagiliaji Mkombilenga wamepata soko la uhakika Jijini Dodoma" alisema Mihayo.

Wakitoa mawasilisho kwa baadhi ya skimu za umwagiliai zilizopo katika kanda nane (8) za umwagiliaji nchini, wakulima wameonekana kutaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo  katika skimu hizo ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa hitaji la  kuongeza mifereji inayopeleka maji katika skimu hizo pamoja na kuisakafia na kuishauri Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa skimu zote ili wakulima wapate uelewa na kutunza skimu jambo ambalo linaweza kusaidia Serikali kufikia lengo la kuweza kuongeza kipato kwa wanachi na kuwepo kwa uhakika wa chakula.

Skimu ya umwagilijai ya Mkombilenga iliyopo katika Kanda ya Mbeya imeibuka kidedea ikifuatiwa na skimu ya Lemkuna ya Kanda ya Dodoma na skimu ya Nyida iliyopo katika Kanda ya Mwanza kushika nafasi ya tatu katika mashindano hayo.

Kongamano hilo la siku mbili lilishirikisha wakulima, wataalam wa kilimo kutoka ngazi za Mikoa, Wilaya, Kanda za Umwagiliaji, Tamisemi na Ofisi za Tume ya Umwagiliaji.

No comments:

Powered by Blogger.