LIVE STREAM ADS

Header Ads

Kiwango cha Mvua chaongezeka Tanzania “rekodi imevunjwa”

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi akizungumza jijini Dar es Salaam kuelezea tathmini ya hali ya hewa kwa mwaka 2019.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi akizungumza jijini Dar es Salaam kuelezea tathmini ya hali ya hewa kwa mwaka 2019. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi akionyesha moja ya picha ya utabiri wa hali ya hewa.


Na Joachim Mushi, Dar
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mwaka 2019 umeweka historia ya pekee kwa kuwa wa nne kihistoria kwa kupata mvua nyingi tangu mwaka 1970. 

Akizungumza Aprili 08, 2020 jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi alisema nchi ilipata wastani wa milimita 1283.5 za mvua sawa na asilimia 125 ya wastani wa mvua ya muda mrefu, yaani tangu mwaka 1981 hadi mwaka 2010. 

Alisema kiwango hicho ni zaidi ya wastani wa mvua ya muda mrefu kwa milimita 256.5 huku maeneo mengi ya nchi yakipata mvua juu ya wastani katika msimu wa vuli na mvua za wastani katika msimu wa masika. 

"Kiwango cha mvua kilichorekodiwa mwezi Oktoba 2019 ni kiwango cha juu kabisa kurekodiwa tangu mwaka 1970. Wastani wa joto nchini kwa mwaka 2019 ulikuwa ni nyuzi joto 23.8 sawa na nyuzi joto 0.9, juu ya wastani wa joto wa muda mrefu (1981-2010) Kiwango hiki cha joto kimechukua nafasi ya nne katika historia ya vipimo vya joto kali tangu mwaka 1970" alieleza Dkt. Kijazi.

Aidha aliongeza kuwa miezi ya Machi na Aprili 2019 iliongoza kuwa na joto la juu ya wastani kwa nyuzi joto 1.1 (Machi) na nyuzijoto 1.6 (Aprili) ukilinganisha na wastani wa muda mrefu.

Alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 1970 na 2019 kumekuwa na matukio kumi na matatu (13) ya mvua za za juu ya wastani katika msimu wa Vuli, na matukio manne (4) tu katika msimu wa Masika na mwaka 2003 ndio ulikuwa na upungufu zaidi wa mvua ukilinganisha na miaka mingine tangu mwaka 1970. 

"Takwimu zinaonyesha kuwa joto la nchi limeendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu kuanzia mwaka 1995. Ambapo joto la usiku (minimum temperature) limeongezeka zaidi ikilinganishwa na joto la mchana (maximum temperature)," alibainisha mtaalam huyo ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

No comments:

Powered by Blogger.