LIVE STREAM ADS

Header Ads

MOROGORO "Serikali kudhibiti mafuriko Mto Furua wilayani Malinyi"

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa Binagi Media Group. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama binagimediagroup@gmail.com
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiongea na Mbunge wa Malinyi Mhe. Antepas Mgungusi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Masele, wakati akikagua sehemu iliyoharibika ya barabara ya Malinyi eneo la Mwembeni katika Kijiji cha Misegese.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Mathayo Masele,akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa kwanza kushoto), alipokagua barabara ya Malinyi eneo la Mwembeni, Kijiji cha Misegese.Barabara hiyo imeharibiwa na mafuriko ya Mto Furua. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Malinyi, Peter Mkaligao.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimweleza jambo Mbunge wa Malinyi (CCM) Mhe. Antepas Mgungusi, baada ya kukagua sehemu ya barabara ya Malinyi eneo la Mwembeni katika Kijiji cha Misegese, iliyoharibika kutokana na mafuriko ya Mto Furua. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Malinyi.Peter Mkaligao.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa pili kutoka kulia), akimsikiliza Mbunge wa Malinyi Mhe. Antepas Mgungusi, baada ya kukagua sehemu ya barabara ya Malinyi iliyoharibika kutokana na kufurika kwa maji ya Mto Furua, eneo la Mwembeni katika Kijiji cha Misegese. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Malinyi ndugu Peter Mkaligao na kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Malinyi Mhe. Mathayo Masele.
Sehemu ya barabara ya Malinyi katika Kijiji cha Misegese eneo la Mwembeni Mkoa wa Morogoro, ikiwa limetengenezewa tuta ili kuzuia maji kupita juu ya barabara hiyo iliyoharibika kutokana na mafuriko ya Mto Furua, huku kazi nyingine za ukarabati wa barabara hiyo zikiendelea.


Na Baltazar Mashaka, Morogoro
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, jana ameamuagiza Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara kwenda wilayani Malinyi kujenga na kurejesha mawasiliano ya barabara kati ya Kijiji cha Misegese na Malinyi Mjini.

Agizo hilo la Mhandisi Kasekenya linatokana na kero ya maji ya Mto Furua kufurika na kupita juu ya barabara iendayo Malinyi mjini, eneo la Mwembeni na kusababisha mawasiliano ya barabara kukatika na kusababisha kero ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Mwembeni,Mhandisi Kasekenya alisema kuwa amefika wilayani humo katika Mkoa wa Morogoro kutembelea na kukagua uharibifu wa barabara ya Malinyi uliosababishwa na maji ya Mto Furua baada ya kina cha mto huo kupungua na kusababisha maji kupita juu ya barabara hiyo.

Alisema serikali itachukua hatua za haraka za kurejesha mawasiliano ya barabara kati ya Kijiji cha Misegese na Malinyi mjini lakini pia kudhibiti mafuriko ya Mto Furua ili kuwaondolea wananchi adha ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa na mazao.

Mhandisi Kasekenya alisema mafuriko ya mto huo yamekuwa kero na kusababisha barabara hiyo kutopitika eneo la Mwembeni katika Kijiji cha Misegese na hivyo kusababisha wananchi kukosa huduma za kijamii zinazopatikana upande wa pili wa mto ambao ni Malinyi mjini.

“Nawashukuru sana wananchi wa Malinyi kwa kujumuika nasi hapa kuelezea changamoto za barabara hii zinazotokana na kufurika kwa Mto Furua, tayari nimeshamtuma Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara kufika hapa na kushirikiana na wataalamu Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro,” alisema.
Naibu Waziri huy wa Ujenzi alimtaka na Mkurugenzi huyo wa Barabara na watalaamu baada ya uharibifu uliotokea kwenye barabara hiyo ya Malinyi ili iweze kupitika majira yote ya mwaka, wahakikishe taratibu za kitaalamu zinafuatwa katika kutengeneza barabara hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mathayo Masele alimshukuru Naibu Waziri huyo wa Ujenzi kwa kufika wilayani hapo na kumweleza kuwa ofisi yake ili kuzuia maji ya Mto Furua kukatiza barabarani imechukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kujenga tuta na kupanda miti na majani,lakini kero imekuwa kubwa sababu ya kupungua kwa kina cha mto huo.

“Nawashukuru TANROADS Morogoro kwa ushirikiano mzuri tangu tatizo hili lilipojitokeza,sisi kama Serikali ya Wilaya tunaahidi kuweka ulinzi wa kutosha baada ya matengenezo ya barabara hii kukamilika na tutahakikisha shughuli za kilimo hazifanyiki ndani ya hifadhi ya barabara na maeneo ya vyanzo vya maji ili kuzuia uharibifu wa barabara hii,” alisema Masele.

Naye Mbunge wa Malinyi (CCM) Mhe. Antepas Mgungusi alisema kutokana na huduma za kijamii kupatikana Malinyi mjini (ng’ambo ya pili ya Mto Furua) wananchi wa Kijiji cha Misegese wanapata tabu sana barabara hiyo inapokuwa haipitiki sababu ya mafuriko ya maji ya mto huo kupita juu ya barabara.

“Tunawaomba TANROADS ikiwezekana mchonge njia ya maji kwenye mto huu pamoja na kuongeza kina chake ili maji yapate njia ya kupita yasifurike tena na sisi tutakuwa macho kuwafichua wote watakaofanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 za hifadhi ya barabara,”alishauri na kuonya Mgungusi.

Aidha Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro,Nkolante Ntije alimweleza Naibu Waziri huyo wa Ujenzi kuwa wamejipanga kuikarabati barabara hiyo kwa kuongeza makaravati sehemu zitakazohitajika pamoja na kuinyanyua barabara hiyo ili maji ya mto huo yasipite tena juu ya barabara, na kwamba utekelezaji unaanza mara moja.
Naibu Waziri Kasekenya alikuwa mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, ili kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mafuriko yanatokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo na kote nchini.

No comments:

Powered by Blogger.