LIVE STREAM ADS

Header Ads

Unyonyeshaji mzuri wasaidia udumavu kupungua Mwanza

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Imeelezwa kuwa kiwango cha udumavu unaosababishwa na kutonyonyeshwa vizuri watoto wachanga kimepungua kutoka asilimia 38.6 hadi asilimia 29.3 mkoani Mwanza.

Hayo yamesemwa na Afisa Lishe Jiji la Mwanza, Joyce Zelamala wakati akizungumzia umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto mchanga katika kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 1/08 hadi 7/08 ya kila mwaka duniani kote,

Zelamala amesema mtoto ambae hajanyonyeshwa maziwa ya mama anaweza kupata tatizo la udumavu wa mwili na akili na mama ambae hakumnyonyesha mtoto wake anauwezekano mkubwa wa kupatwa na saratani ya matiti.

Amesema kuna faida kubwa ya mama kumnyonyesha mtoto maziwa yake mwenyewe kwa kuwa yanasaidia ukuaji wa jumla wa mtoto,ukuaji wa ubongo wa mtoto na pia maziwa ya mama humkinga mtoto na maradhi mbalimbali ya utotoni.

"Katika maziwa ya mama kuna vitatu vya msingi ikiwa ni pamoja na protini, mafuta, vitamini A, B, E, C na potassium ambavyo humsaidia mtoto kuwa na kinga ya kupambana na magonjwa hivyo ni kosa kubwa mama akiacha kumnyonyesha mtoto mchanga kwa kuwa hivyo vyote havipatikani kwenye maziwa mengine" amesema Zelamala.

Akizungumzia upande wa Sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 ambayo inatoa likizo ya uzazi ya siku 84 kwa mama aliyejifungua, Zelamala amewataka waajiri kuheshimu sheria hiyo ambayo inampa mama muda wa kunyoshesha mtoto kwa ukaribu ndani ya miezi mitatu mfululizo.
Naye Holo Masanja mama wa mtoto mmoja mkazi wa jijini Mwanza amewashukuru watoa tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwanza Sekou Toure kwa kuwapatia elimu ya umuhimu wa kunyonyesha mara baada ya kujifungua.

"Kiukweli mwanzoni mimi sikujua umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto na nimekuja kupata elimu hiyo baada ya kujifungua pamoja na mambo mengi. Nesi alitusisitiza tuhakikishe tunawanyonyesha watoto miezi sita mfululizo ili waweze kukua vizuri na kuwa na afya njema" amesema Masanja.

Kauli mbiu ya Siku ya Unyonyeshaji Duniani mwaka huu 2021 ni "Kulinda Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama ni Wajibu Wetu Sote".
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya WHO limewataka wanawake wanaonyonyesha kupata chanjo na kuendelea kunyonyesha kama kawaida kwa kuwa hakuna chanjo yoyote iliyothibitishwa kuleta athari kwa mtoto atakayenyonya maziwa ya mama aliyechanjwa.
Na Tonny Alphonce, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.