LIVE STREAM ADS

Header Ads

Waziri Jafo apokea Ripoti ya Uchafuzi Mto Mara

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Online Media. Mawasiliano 0757 43 26 94 ama ripotabmg@gmail.com
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Kamati ya kitaifa ya watu 11 iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu ya Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) vimetofautiana kwenye taarifa ya uchunguzi wa kilichodaiwa uchafuzi wa Mto Mara.

Wakati taarifa ya uchunguzi uliofanywa na LVBWB ikitaja chanzo cha uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika mto Mara kuwa ni kiwango kikubwa cha mafuta, grisi na kukosekana kwa hewa ya oksijeni kwenye maji, taarifa ya Kamati iliyoundwa na Waziri Jafo imesema sababu ya uchafuzi huo ni nguvu za asili, kinyesi cha mifugo na uozo wa mimea.

Waziri Jafo amepokea taarifa hiyo mjini Musoma Machi 19, 2022 akieleza kuridhishwa nayo, huku akiiongezea Kamati hiyo muda wa siku mbili kuandaa na kuwasilisha taarifa kamili ya uchunguzi huo na mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo iliyotoa.

Machi 12, 2022, Waziri Jafo aliunda Kamati ya Kitaifa ya watu 11 kutoka sekta mbalimbali kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha kilichodaiwa ni uchafuzi wa maji na vifo vya samaki katika Mto Mara.

Taarifa ya uchunguzi uliofanywa na LVBWB ilitolewa na Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Renatus Shinhu, Machi 12, 2022 na taarifa ya Kamati ya Watu 11 imewasilishwa leo kwa Waziri Jafo na kiongozi wa Kamati hiyo, Profesa Samweli Mayele.

Tayari mamlaka zimeshazuia wananchi katika vijiji jirani kutumia maji ya mto huo kwa mahitaji yoyote baada ya hali ambayo ilisababisha harufu kali ya uvundo mtoni.

Tukio la uchafuzi wa mto Mara unaotiririsha maji kwenye Ziwa Victoria, liliripotiwa hivi karibuni katika eneo la Kirumi darajani.
Imeandikwa na Mara Online

No comments:

Powered by Blogger.