LIVE STREAM ADS

Header Ads

Serikali yaendelea kuboresha huduma kwa watoto njiti, kukabiliana na vifo

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO), watoto milioni moja hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kuzaliwa kabla ya miezi tisa huku shirika hilo likibainisha kuwa kwa kila watoto 10 wanaozaliwa, mmoja huzaliwa kabla ya wakati (njiti).

Aidha shirika hilo pia linaeleza kuwa robo tatu ya vifo hivyo vinaweza kuzuilika ikiwa afua mbalimbali zitachukuliwa ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya ikiwemo kuwasaidia watoto njiti (wanaozaliwa chini ya wiki 37).

Katika kukabiliana na vifo hivyo, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH ili kuwajengea uwezo watumishi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo kuwasaidia watoto njiti katika vituo vya afya na hospitali nchini.

Hili linathibitishwa na Salma Ramadhan (23) mkazi wa Kijiji cha Iboja Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambaye mwezi Agosti mwaka huu alijifungua mtoto wake wa pili akiwa na ujauzito wa miezi saba ambapo alihudumiwa huduma katika Kituo cha Ukune.

"Nilijifungua mtoto mtoto mdogo sana akiwa na uzito wa kilo moja ambapo madaktari walinihudumia vizuri ambapo nilikaa hospitalini kwa muda wa mwezi mmoja na nusu nikaruhusiwa kutoka" amesema Salma.

Salma ameongeza kuwa akiwa katika kituo cha afya Ukune, madaktari pia walimwelekeza jinsi ya kumbeba mtoto wake kwa njia ya kangaroo ili anendelee kupata joto la mwili na sasa anaendelea vizuri ambapo anaelekea kutimiza miezi miwili na uzito pia umeongezeka hadi kilo mbili.

"Nafurahi sana kumuona huyu maana maana nilipojifungua nikiwa na miezi saba, sikutarajia kama atafikia hatua hii. Naishukuru sana Serikali kwa kushirikiana na wadau kwa kuleta hapa hii huduma ya kuwasaidia watoto njiti" amesema Salma.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ukune, Dkt. Elikana Lubango amesema mafunzo yaliyotolewa na Serikali kupitia mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH wameimarisha ufaniki wa watumishi kuwahudumia watoto wachanga ambapo kituo hicho kimeanzisha wodi maalumu ya watoto njiti (Kangaroo Mother Caer) na hivyo kuondoa adha ya kuwapa rufaa kwenda hospitali ya Wilaya Kahama.

Naye Mratibu Msaidizi Afya, Uzazi, Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga, Hellen Kasakenta amesema katika kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuimarika katika vituo vya afya, wamekuwa wakiwatumia madaktari bingwa kuwajengea uwezo watumishi hatua ambayo imeleta tija hususani katika huduma za uzazi.

Jitihada zilizofanywa na Serikali kwa kushirikiana na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH na kuimarisha huduma za uzazi katika kituo cha afya Ukune zimekuwa miongoni mwa afua za kupambana na vifo vya uzazi kwa wanawake na watoto wakiwemo njiti na hivyo kuleta furaha kwa wanawake wengi hususani vijijini akiwemo Salma.

Inaelezwa kuwa wanawake wanajifungua chini ya umri wa miaka 18, wanaopata uchungu mapema, wenye maradhi katika njia ya mkojo, wenye matatizo katika maumbile ya mfumo wa uzazi na kujifungua mara kwa mara katika kipindi kifupi wako kwenye hatari ya kujifungua mtoto njiti.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mmoja wa wanawake kutoka Kijiji cha Iboja Halmashauri ya Ushetu wilayani Kamahama, Salma Ramadhan akiwa amembeba mwanaye kwa njia ya kangaroo.
Mganga Mfawithi Kituo cha Afya Ukune kilichopo Ushetu wilayani Kahama, Dkt. Elikana Lubango.
Mratibu Msaidizi Afya, Uzazi, Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga, Hellen Kasakenta.
PIA SOMA>>> HUDUMA ZA UZAZI

No comments:

Powered by Blogger.