LIVE STREAM ADS

Header Ads

Ushirikiano baina ya Serikali na USAID Afya Yangu- RMNCAH wazaa matunda Sikonge, Tabora

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, zimesaidia kukabiliana na vifo vya wamama wajawazito na watoto katika Kituo cha Afya Kitunda

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dkt. Faudhi Ulungu amesema kwa mwaka kulikuwa na vifo 12 vitokanavyo na uzazi lakini baada ya watumishi kujengewa uwezo hususani kwenye eneo la kumhudumia mama mjamzito na upasuaji wamefanikiwa kuondoa kabisa vivo hivyo.

“Tulikuwa tunapata vifo vya wamama wajawazito hadi 12 kwa mwaka lakini baada ya Serikali kwa kushirikiana na mradi wa USAID Afya Yangu- RMNCAH kutujengea uwezo, tumepunguza vifo hivyo hadi sifuri” amesema Dkt. Ulungu.

Aidha Dkt. Ulungu amebainisha kuwa kati ya akina mama 10 wanaojifungua kwa siku katika Kituo hicho, akina mama watatu wanajifungua kwa upasuaji ambapo sasa hawalazimiki kuwapa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya Sikonge iliyopo umbali wa takribani kilomita 200.

“Kwa siku tunazalisha akina mama 10, kwa wiki wanafika 70 na takwimu mpya tulizonazo wanafika 418 kwa mwezi” amesema Dkt. Ulungu.

Dkt. Ulungu ameongeza kuwa elimu inayotolewa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii imesaidia kubadili mtazamo kwa wanawake wajawazito na hivyo kutambua umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya afya.

Nao aadhi ya wananchi akiwemo Luhende Lucas wamesema upatikanaji wa huduma za upasuaji hususani kwa wanawake wajawazito katika Kituo cha Afya Kitunda umeondoa adha waliyokuwa wakiipata na hivyo kuomba Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya kaika Kituo hicho.

Kituo cha Afya Kitunda wilayani Sikonge kinahudumia wakazi wa Kata ya Kitunda na maeneo jirani ikiwemo Itigi mkoani Singida, Chunya mkoani Mbeya na Inyonga mkoani Katavi, hivyo kuimarika kwa huduma za afya hususani upasuaji kumeondoa adha kubwa kwa wananchi.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kitunda kilichopo Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Dkt. Faudhi Ulungu akifuatilia maendeleo ya watoto waliozaliwa kabla ya miezi tisa (watoto njiti) katika Kituo hicho. 
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kitunda kilichopo wilayani Sikonge, Dkt. Faudhi Ulungu akieleza namna upatikanaji wa huduma za upasuaji ulivyosaidia kuondoa adha kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya Sikonge takribani kilomita 200 kufuata huduma hiyo.
Mwonekano wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Kitunda wilayani Sikonge.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kitunda kilichopo Wilaya ya Sikonge, Dkt. Faudhi Ulungu (kulia) akiwa kwenye maandalizi ya kufanya upasuaji.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.